Mkurugenzi mkuu NBS, Dk. Albina Chuwa
 
PATO la Taifa (GDP) kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2015, limetajwa kukua kwa kasi ya asilimia 6.3 ikilinganishwa na asilimia 5.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2014.

“Hii ina maana gani kwa mwananchi wa kawaida? Ni kwamba Serikali imeendelea kutoa huduma zake mbalimbali kwa wananchi wake kama iliyopangwa katika sekta zote za kiuchumi,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Dk Chuwa alitaja sekta hizo kuwa ni za kilimo, uzalishaji viwandani, elimu, afya, ujenzi, mawasiliano, maji, umeme, uchimbaji wa madini pamoja na huduma zingine zinazotolewa na Serikali.

Alisema katika kipindi hicho, viashiria vingine vya kiuchumi vinaonesha kutoyumba kwa uchumi wa nchi, kwani thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi iliongezeka kwa asilimia 3.3.
Dk Chuwa alisema thamani ya bidhaa na huduma zilizoagizwa kutoka nje zilipungua kwa asilimia 0.58 ambapo malighafi na bidhaa za walaji ziliagizwa kutoka nje ya nchi katika kipindi hicho cha Julai hadi Septemba zilipungua ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2014.

“Hii ni dalili nzuri kwa uchumi unaokua kwa kuwa bidhaa nyingi na huduma zitakuwa zinapatikana ndani ya nchi. Na hii ndio sera ya uchumi jumla kwa nchi yoyote duniani,” alisema Dk Chuwa.
Dk Chuwa alisisitiza kuwa thamani ya Pato la Taifa kwa bei za miaka husika katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba 2015 ni Sh trilioni 71.7 sawa na ongezeko la asilimia 6.9.
“Kama tunakumbuka katika robo ya kwanza na ya pili ya mwaka 2015 Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 6.5 na 7.9, kwa mtitiriko huo,” alisema.

Alisema kutokana na takwimu za Pato la Taifa kwa kipindi cha Januari hadi Septemba 2015 kama hakutakuwa na misukosuko ya kiuchumi duniani inategemewa kuwa makadirio tarajiwa yatafikiwa.
Shughuli za kiuchumi Aliitaja shughuli za kiuchumi ambazo zilikua kwa kasi kubwa ni ujenzi kwa asilimia 17.6, uchukuzi na uhifadhi (10.6%), uendeshaji serikali na ulinzi (10.6%) na uchimbaji madini na kokoto asilimia 8.0.

Akizungumzia uendeshaji wa Serikali na Ulinzi, Dk Chuwa alisema zilikuwa kwa asilimia 10.6 kutoka asilimia 10 mwaka 2014. Alisema ukuaji huo ulitokana na ajira mpya kwa wafanyakazi wa umma na shughuli za utunzaji wa amani wakati wote wa kipindi cha uchaguzi.
Aliongeza kuwa shughuli za kiuchumi za kilimo, uzalishaji viwandani, umeme, biashara za jumla na rejareja, habari na mawasiliano, fedha na bima zilikua kwa kasi ya chini ya asilimia 3.0 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2014.

Akizungumzia ukuaji wa baadhi ya shughuli za kiuchumi katika kipindi hicho, Dk Chuwa alisema kilimo cha mazao kilikua kwa asilimia 2.6 kutoka asilimia 3.1 mwaka 2014, shughuli ndogo za uzalishaji mazao ya kilimo, zao la mahindi lilichangia asilimia 23.

“Uzalishaji wa mahindi ulikuwa tani 2,148,000 ikilinganishwa na tani 2,092,000 katika kipindi kama hicho mwaka 2014,” alisema Dk Chuwa na kuongeza kuwa ufugaji uliongezeka kwa asilimia 3.4 kutoka asilimia 2.1.

Shughuli za uchimbaji madini, mawe na kokoto ziliongezeka kwa kasi ya asilimia 8.0 kutoka asilimia 5.2. Katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2015 uzalishaji wa dhahabu ambayo inachangia asilimia 89 ya madini yote ilikuwa kilo 10,315 ikilinganishwa na kilo 10,137 za mwaka 2014.
“Kuongezeka kwa uzalishaji wa dhahabu kulichangiwa na bei nzuri ya bidhaa hiyo katika soko la dunia,” alisema na kuongeza kuwa uzalishaji wa madini kama tanzanite, almasi na shaba ulikuwa mdogo ukilinganisha na uzalishaji wa madini hayo mwaka 2014.

Kwa upande wa uzalishaji wa bidhaa za viwandani, Dk Chuwa alisema zilikua kwa kasi ya asilimia 3.6 kutoka asilimia 6.3. Kasi hiyo ndogo ilitokana na ongezeko dogo la uzalishaji wa bidhaa za yakula, vinywaji na bidhaa za tumbaku.
Katika kipindi hicho uzalishaji wa bidhaa za nguo, dawa na bidhaa za plastiki ulipungua pia. Shughuli za fedha na bima katika kipindi hicho zilikua kwa asilimia 6.6 kutoka asilimia 9.4.
Dk Chuwa alisema sababu ya ukuaji huo ni kuongezeka kwa kiwango cha amani kutoka Sh trilioni 14.8 mwaka 2014 hadi Sh trilioni 16.8, kuongezeka kwa mikopo kutoka Sh trilioni 11.7 mwaka 2014 hadi Sh trilioni 14.3 mwaka 2015.

Post a Comment

 
Top